Jukwaa la Uziduaji 2019 lafanyika Dodoma, wadau walia na umasikini

Dodoma, Tanzania

Na Mwandishi wa JARET

KONGAMANO la uziduaji la sekta ya rasilimali za madini, gesi na mafuta limefanyika mjini Dodoma likiwashirikisha wadau mbalimbali katika sekta hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania likiwa na lengo la kujenga ubia wa pamoja katika sekta hiyo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo, Mratibu wa HakiRasilimali Tanzania, Racheal Chagonja, amesema kadri muda unavyokwenda jamii imekuwa ikitarajia kupata naamufaa makubwa ya madini lakini hali imekuwa kinyume kutokana na jamii ya wananchi wanaozunguka migodi wakiishi katika umaskini, wakiwa hawana ajira, hivyo kuongezeka kwa pengo baina ya walia nacho na wasio kuwa nacho.

Alisema kwa hali hiyo serikali na wadau mbalimbali katika sekta hiyo wanapaswa kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika na utajiri huo wa madini.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza katika kongamano hilo alisema sekta ya madini imekuwa na manufaa makubwa ilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kuweka mikakati mizuri ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za madini, gesi na mafuta.

Serikali inataka nchi hii pamolja na watu wake wafaidike na uwepo wa rasilimali za madini, ndiyo maana tumefanya mabadiliko ya sheria ili serikali imiliki asilimia 16 ya hisa katika makampuni yanayokuja kuwekeza kwenye sekta ya uziduaji;-Naibu Waziri wa Madini, Mh. Stanslaus Nyongo


Wakati Serikali ikielezea mikakati yake katika sekta ya uziduaji, bado wadau wamekuwa wakiendelea kulalamika kuwepo na chanamoto ambazo walieleza kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara na wachimbaji wadogo katika sekta hiyo.

Kaanaely Minja mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, alisema wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupandishiwa gharama za tozo la kibali cha ununuzi wa vilipuzi kutoka Sh 20,000 hadi Sh 100,000, huku akilaani kitendo cha askari kuwapekuwa wanawake kwa kuwavua nguo kuhofia utoroshaji wa madini hayo.

“Kama sisi wanawake tukiingia ndani ya ukuta wa machimbo ya Tanzanite, wakati wa kutoka huwa tunafanyiwa udhalilishaji mkubwa, hakuna tena haki ya faragha…, mkifika kwenye foleni mnaingia kwenye kichuma kimoja wanawake wanne hadi sita na kuamuriwa kuvua ngua zenu ili mbaki utupu na kuanza kukaguliwa,”alisema.

Aidha mmoja wa wadau wa sekta ya madini kutoka nchini Kenya, Angela Mutoto, aliyeshiriki kongamano hilo alisema amejifunza mambo mengi ikiwemo changamoto wanazopata wakazi wa Mkoa wa Geita kutokana na uwepo wa mgodi mkubwa wa uchimbaji dhahabu.