Uzalendo wetu utatupa tunachotaka kwenye rasilimali zetu?

By Romana Celestine

Hakuna shaka yoyote kwamba mafanikio ya kiuchumi ambayo Tanzania imefanikiwa kuyapata katika kipindi cha miaka 20 iliyopita; ambapo uchumi umekua ukikua kwa wastani wa asilimia sita kwa mwaka, yalichagizwa pia na sekta ya uziduaji.

Kwa sababu nchi yetu bado imejaaliwa utajiri wa rasilimali hizi za asili kama madini, mafuta na gesi ambazo ndiyo kwa pamoja hutengeneza sekta nzima ya uziduaji, ni wazi kwamba bado kuna uwezekano mkubwa wa kufaidika zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Ili kufikia malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) pamoja na malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, mchango wa sekta hii ya uziduaji utakuwa muhimu kwa sababu ya ukubwa wake na mawanda yake ya kiuchumi .

Mimi ni raia wa Tanzania na Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka wazi kwamba “Kila raia ana wajibu wa kulinda rasilimali za taifa lake”. Ni kwenye muktadha huo wa kikatiba ndiyo hasa napata nguvu ya kujenga hoja ninazotaka kuzijenga kupitia makala haya.

Mwanzoni mwa mwezi ujao, kati ya Novemba 4 hadi 8 mwaka huu, asasi za kiraia nchini zitakutana jijini Dodoma kwenye tukio maarufu lijulikanalo kwa jina la Wiki ya Asasi za Kiraia (Wiki ya Azaki).

Nafahamu kwamba asasi zinazojihusisha na masuala ya uziduaji pia zitakutana chini ya uratibu wa asasi inayojulikana kwa jina la HakiRasilimali. Kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, masuala anuai ya sekta hiyo yatajadiliwa kwa kina na washiriki kwa lengo la kuona nchi yetu inafaidika zaidi na utajiri wake wa rasilimali.

Mkutano huo wa wadau wa tasnia ya uziduaji unajulikana kwa jina la Jukwaa la Uziduaji na huwa ni sehemu ya mijadala inayohanikiza Wiki ya Azaki. Ni matumaini yangu kuwa, kama ilivyokuwa mwaka jana na mwaka juzi, mwaka huu pia wajumbe watajadili kwa kina mambo muhimu kuhusu tasnia yao

Ni muhimu kufahamu kwamba Jukwaa za Uziduaji la mwaka huu linafanyika katika mazingira ya serikali ya awamu ya tano ambayo imejipambanua kwa kutaka kuona Watanzania wanafaidika kutokana na utajiri wa rasilimali zao.

Zimeundwa sheria mpya na nyingine kufanyiwa marekebisho kwa lengo hilo muhimu la kuhakikisha Watanzania wanafaidi utajiri wao wa rasilimali. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba Tanzania si kisiwa na yanayoendelea kwa kiasi kikubwa yana athari katika uchumi mpana wa dunia nzima.

Ndiyo sababu, washiriki wa mkutano huo chini ya HakiRasilimali wanatakiwa kujadili kwa kina kuhusu ni kwa kiasi gani sheria zetu za kizalendo zilizopitishwa bungeni zinaathiriwa na mfumo wa kidunia unaotawala sekta ya uziduaji.

Je, kupitia sheria zetu tutafaidika vipi na mfumo huu wa kidunia. Kuna fursa zipi za kunufaika? Kuna changamoto zipi za kupambana nazo na kama kuna mafunzo ya kujifunza, ni muhimu yakafunzwa kutokana na sheria zile zilizopitishwa mwaka 2017

Hoja za namna hii ni muhimu kujadiliwa kwa kina kwa sababu Tanzania si kisiwa. Nchi yetu iko ndani ya mfumo wa kiuchumi wa dunia na huko nje kuna mengi ya kujifunza na kujielekeza ili nchi yetu iweze kupata faida ambazo sote tunazitarajia.

Inafahamika kwamba katika sekta hii ya uziduaji kuna lawama ambazo serikali na sekta binafsi zimekuwa zikipata mara kwa mara. Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa urasimu na kujifanyia maamuzi pasipo kushirikisha wadau wake huku sekta binafsi kwa maana ya kampuni za madini imekuwa ikishutumiwa kwa kukwepa kulipa kodi, kutokuwa waaminifu na kutounganisha sekta hii na nyingine za kiuchumi.

Kwa maoni yangu, jambo moja ambalo linaweza kufanikisha malengo ya serikali, asasi na sekta binafsi (ambazo kwa bahati nzuri nimeambiwa zote zitashiriki katika Jukwaa za Uziduaji 2019), ni kuweka mazingira ya kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano wa karibu.

Na ushirikiano huu hautakiwi kuishia hapa nchini pekee kwa sababu jambo hili linahusisha dunia nzima. Katika wakati ambao Tanzania na Uganda zinashirikiana katika mradi wa bomba la mafuta, hakuna namna ambayo ushirikiano wa nchi jirani unaweza kupuuzwa.

Ni jukumu la wadau wa sekta hii watakaokutana Dodoma kujadiliana pia kuhusu mapengo yaliyopo katika sera na utekelezaji wake kwa sababu wakati mwingine sera zinakuwa nzuri lakini utekelezaji unakuwa mbovu.

Katika uzoefu wangu wa kufuatilia sekta hii ya uziduaji, nimejifunza kwamba uzalendo wa rasilimali pekee hautoshi kusaidia nchi kufaidika na utajiri wa rasilimali ilizojaaliwa na Mungu.

Uzalendo na sheria nzuri ni vitu muhimu lakini ni muhimu zaidi kukutana na kuangalia yalipo mapungufu, kujenga ushirikiano na kuaminiana miongoni mwa wadau wa sekta husika pamoja na kuwa macho katika kuangalia nini kinaendelea kwingineko katika tasnia hii ya uziduaji.

Katika mfumo huu wa uchumi wa kidunia kwa sasa, itakuwa ni makosa kufanya mambo kana kwamba nchi yetu ni kisiwa kilichojitenga na dunia. Ndiyo sababu, kama kuna kitu nakitaraji kutoka katika Jukwaa za Uziduaji mwaka huu, ni kwa washiriki kujadiliana kwa kina, kuja na majawabu ya kujenga na kutuvusha kutoka tulipo sasa na kwenda hatua nyingine.

Na hili litafanikiwa kwa kujenga mtandao imara wa ushirikiano na kuaminiana baina ya serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wananchi ambao Katiba ya Tanzania inawataja kuwa ndiyo hasa wenye rasilimali hizo.