Tunahitaji sheria moja kufaidika na uwekezaji kwenye uziduaji

Na Hezron Okwanga

Tunaishi katika zama muhimu sana katika sekta ya uziduaji hapa nchini. Hizi ni zama za uzalendo wa kirasilimali; ambazo zimechagizwa na namna Serikali ya Rais John Magufuli, ilivyoamua kusimamia sekta hii.

Tangu kuingia madarakani takribani miaka minne iliyopita, serikali ya Rais Magufuli si tu kwamba imebadili upepo kwa kutengeneza sheria mpya za kizalendo za kulinda utajiri wa rasilimali za Watanzania, lakini pia umetoa mwelekeo kwamba mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa huku nyuma.

Tumeshuhudia mabosi wa kampuni kubwa za sekta ya uziduaji wakija Tanzania kuzungumza na viongozi wetu; jambo ambalo halikuwa la kawaida kwani huko nyuma viongozi wetu ndiyo walikuwa wakiwafuata wakubwa hawa.

Hata hivyo, kama kuna jambo la msingi ambalo linapaswa kufanyika ni kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na sheria moja ambayo itahakikisha nchi inanufaika kiuchumi kupitia uwekezaji unaofanywa na kampuni za uziduaji.

Katika lugha ya Kiingereza, neno linalotumika ni local content, na linaeleza ni kwa kiasi gani serikali na wananchi wanaweza kufaidika moja kwa moja kupitia uwekezaji unaofanywa kupitia sekta hiyo.

Tunapozungumzia kufaidika huku kwa jamii husika katika sekta sekta ya uziduaji – yaani madini, gesi na mafuta, tunazungumzia masuala kama vile ajira, mitaji na huduma nyingine ambazo kampuni za uziduaji huhitaji kwa matumizi yake.

Kumekuwa na mifano mingi sana kuhusu namna gani Tanzania na Watanzania wamekuwa wakipoteza fursa ya kupata zaidi kupitia utajiri wake kutokana na kukosa sera moja thabiti ya kutazama namna tunavyoweza kufaidika kupitia uwekezaji huu.

Kumekuwa na kilio kuhusu namna gani wafanyakazi wa kigeni na kizalendo katika kampuni za uziduaji wamekuwa wakipata huduma za vyakula, vifaa tiba, usafiri, mafuta, vinywaji na mambo mengine kutoka nje ya Tanzania ilhali Watanzania wangeweza kuwezeshwa na kutoa huduma hizo

Malalamiko makubwa kuhusu sekta ya uziduaji hapa nchini yamekuwa kwamba kampuni hizo zimeshindwa kufungamanisha sekta hiyo na sekta nyingine nyeti kwenye ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kwa mfano, kama kampuni hizi zikilamishwa kupitia sheria na kuwekwa utaratibu mzuri, zinaweza kuanza kununua vyakula kutoka kwa wazalishaji wa Tanzania na jambo hilo litafaidisha wakulima, wavuvi na wafugaji wa nchi yetu.

Jambo lolote lenye faida kwa wakulima wa Tanzania ni la muhimu kiuchumi kwa sababu zaidi ya nusu ya wananchi wa taifa hili ni wakulima na hivyo watu wetu wengi watafaidika kiuchumi na hatua hizo.

Jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na asasi za kiraia, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kuhusu serikali ni kwamba mara nyingi imekuwa ikihodhi mchakato mzima wa kutengeneza sheria zenye faida kwa makundi yote.

Mapema mwezi ujao, kati ya Novemba 4 mpaka 8 mwaka huu, asasi za kiraia nchini zinazojihusisha na sekta ya uziduaji chini ya uratibu wa taasisi ya HakiRasilimali zitakutana jijini Dodoma kwenye mkutano wa Jukwaa la Uziduaji ambako ni matarajio yangu kwamba jambo hili litazungumzwa kwa kina.

Kwa bahati nzuri, tangu kuanzishwa kwake miaka miwili iliyopita, Jukwaa la Uziduaji limekuwa likikutanisha pande zote nne muhimu; serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wananchi wa kawaida, na ni matarajio yangu kwamba jambo hili litatazamwa kwa kina.

Tasnia ya uziduaji inahusu maeneo tofauti kama vile madini, gesi na mafuta na ni matarajio ya wengi kwamba wadau watakaa chini kwa pamoja na kujadiliana kwa kina kuhusu nini kifanyike kwenye kuhakikisha Watanzania kwa ujumla wao wanafaidika na uwekezaji huu.

Kwa kuzingatia uzoefu wa kwingineko duniani, nchi ambazo zina sera nzuri ya kufaidika na uwekezaji kwenye uziduaji ni zile zenye sheria moja mtambuka katika tasnia nzima. Haisaidii kuwa na sheria moja kwa gesi, nyingine kwa madini na nyingine kwa mafuta.

Jambo lingine ambalo ni muhimu kulitazama katika muktadha wa sasa linahusu suala zima la huduma ambazo kampuni za uziduaji hutoa kwa jamii zinazozunguka maeneo yenye utajiri wa rasilimali zinakofanya shughuli zake.

Katika makubaliano yaliyotangazwa karibuni baina ya serikali na kampuni ya kimataifa ya Barrick, inaonekana kuwa kampuni hiyo inataka huduma hizo zichukuliwe kuwa ni sehemu ya gharama za uendeshaji na si misaada kama inavyoonekana kwa wengi.

Sote tunafahamu kuhusu hospitali, shule, madaraja, malambo ya maji na visima ambavyo vimekuwa vikijengwa na kampuni za uziduaji katika maeneo yanakofanya shughuli zao kama mchango wao kwa jamii hizo.

Kwa tu wengi, jambo hilo lilikuwa likionekana kama la hiyari lakini sasa inaonekana halitakuwa namna hiyo na linaweza kuwa na athari zake kwenye uchumi. Katika nchi nyingi duniani, huduma hizo huchukuliwa kama sehemu ya gharama za uendeshaji na ni muhimu nasi kuangalia tunataka kuliona namna gani jambo hili.

Katika ufaidikaji huu wa uwekezaji katika sekta ya uziduaji kumekuwapo na tatizo la kudhani kwamba tunaposema wananchi tunamaanisha wote ni wa aina moja. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kwamba kuna makundi kama wanawake na walemavu ambao huachwa nyuma zaidi kuliko wanaume na walio wazima na lazima jambo lolote la kufaidisha wananchi lizingatie makundi haya maalumu.

Kama kuna jambo ambalo Watanzania wamejifunza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita ni kwamba tasnia ya uziduaji ina mchango muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Tanzania kwa ujumla.

Katika kipindi ambacho uchumi wetu umekuwa ukikukua kwa kiwango cha asilimia sita kwa takribani miongo miwili; pasi na shaka yoyote ukuaji huo ulichagizwa na sekta ya uziduaji.

Hata hivyo, kama ambavyo serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikionyesha, huu si wakati wa kulewa sifa na kubweteka; badala yake, huu ni wakati wa kukaa chini na kutazama kwa kina zaidi namna ambavyo tunaweza kufaidika zaidi na utajiri huu.

Jambo moja la wazi na yakini katika sekta ya uziduaji ni kwamba utajiri huu wa rasilimali unakwisha. Sio mchanga wa ardhini au maji ya baharini ambayo unajua vitaendelea kuwepo daima dawamu. Madini, gesi na mafuta ni utajiri wa muda na hatutaka umalizike wote pasipo kuwa na cha kuwaonyeshea wale watakaokuja baada yetu.